Thursday, June 21, 2012

SITTI MTEMVU AMSAIDIA SH. 500,000 MSICHANA HAPPINESS KAAYA MLEMAVU ANAYEISHI NDANI KWA MIAKA 22.

 

  MWANAFUNZI wa Chuo Kukuu cha North Texas cha Marekani, Sitti Mtemvu (kushoto), akitoa msaada wa sh. 500,000 kwa msichana Happines Kaaya (22), aliyezaliwa akiwa mlemavu, katika hafla iliyofanyika Machimbo, Temeke, Dar es Salaam juzi
Sitti akitoa msaada mwingine wa sh. 200,000 kwa mtu mwenye ulemavu, Nassoro Tayari mkazi wa Buza jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya kununulia vipuri vya kutengenezea baiskeli yake.

Na Richard Mwaikenda
MWANAFUNZI wa Chuo Kukuu cha North Texas, Marekani, Sitti Mtemvu, ametoa msaada wa sh. 500,000 kwa msichana Happines Kaaya (22), aliyezaliwa akiwa mlemavu.

Msaada huo alikabidhi kwa mama mzazi wa Happiness, Khadija Msuya katika hafla iliyofanyika kwenye chumba  wanachoishi  eneo  la Machimbo, Temeke, Dar es Salaam juzi.

Siti ambaye pia ni Mkurugenzi wa  Mtemvu Foundation, alisema kuwa ameamua kutoa msaada huo baada ya kuguswa na taarifa za msichana huyo alizozisoma kwenye mafaili ya mfuko huo, zilizopo Temeke, Dar es Salaam.

"Taarifa za msichana huyu, zilinigusa mno kuliko wengine, kiasi cha kuamua kuanza kutoa msaada kwa Happiness aliyezaliwa akiwa mlemavu na analelewa mamake kwa shida,"alisema Siti.

Siti ambaye ni mtoto wa kwanza wa Mbunge wa Jimbo la Temeke, Abbas Mtemvu, alisema kuwa fedha alizizitoa ni sehemu ya mapato yanayotokana na bajaji zake tatu zinazofanya biashara ya kubeba abiria jijini  Dar es Salaam.

Alisema kuwa Bajaji hizo alizinunua kutoka na na fedha alizolipwa baada ya kushiriki kwenye filamu moja nchini Marekani anakosoma.

"Sitoishia kutoa msaada kwa msichana huyo, bali nina imani Mungu akinijalia nitaendelea kutoa msaada kwa yatima na watu wengine wanaoishi kwenye mazingira magumu"alisema Siti.

Mama mzazi wa Happiness, Khadija, alishukuru kupata msaada huo kutoka kwa Sitti, ambao alidai utamsaidia sana kupunguza baadhi ya matatizo yanayomkabili.

Alisema kuwa mtoto huyo ambaye alimzaa akiwa na ulemavu, hana uwezo wa kutembea ambapo hata kula chakula ni vigumu inabidi alishwe na kumsaidia wakati wa kujisaidia.

Alidai kuwa Baba mzazi wa Happiness, Joel Kaaya  alimtelekeza yeye na mwanawe ambapo mpaka sasa haijulikani aliko.

Msuya alitoa wito kwa watanzania wengine kujitokeza kusaidia hata ikiwezekana kumnunulia happiness kiti cha magurudumu kitakachorahisisha kumpeleka Hospitali na hata kutoka nje kucheza na wasichana wenzie.
Pia siku hiyo, Siti alitoa msaada mwingine wa sh. 200,000 kwa mtu mwenye ulemavu, Nassoro Tayari mkazi wa Buza jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya kununu vipuri vya kutengenezea baiskeli yake.

Rais Kikwete akutana na Viongozi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na shirika la nyumba mjini Dodma leo.

 

Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akiwa katika mkutano na viongozi wa mifuko ya hifadhi ya Jamii na Shirika la Nyumba la taifa ikulu mjini Dodoma leo.Katika kikao hicho Mheshimiwa Rais aliwapa changamoto viongozi hao  kuunganisha nguvu na kubuni mikakati itakayowezesha kuwapatia watumishi wa umma nyumba za kuishi. PICHA NA FREDDY MARO
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akisisitiza jambo wakati akiongea na mkurugenzi mkuu wa PPF Bwana William Eriyo mjini Dodoma leo baada ya kikao maalumu na viongozi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na shirika la Nyumba .
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na shirika la Nyumba la Taifa mara baada ya kikao maalumu kilichofanyika ikulu mjini Dodoma leo. viongozi Wengine waandamizi w aliohudhuria kikao hicho Naibu Waziri wa Ardhi Goodluck ole Medeye(watatu kushoto),Katibu Mkuu kiongozi Balozi Ombeni Sefue(Wanne kushoto),Gavana wa Benki Kuu Professa Beno Ndulu(kulia) na naibu katibu Mkuu Hazina Dr.Servacius Likwelile(kushoto). Katika kikao hicho Mheshimiwa Rais aliwapa changamoto viongozi hao  kuunganisha nguvu na kubuni mikakati itakayowezesha kuwapatia watumishi wa umma nyumba za kuishi.
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akiagana na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa NHC Bwana Nehemiah  Mchechu mara baada ya kikao maalumu kilichofanyika ikulu mjini Dodoma leo(picha na Freddy Maro)
Mkurugenzi Mkuu wa NSSF Dr.Ramadhani Dau akiteta Jambo na Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete ikulu mjini Dodoma leo