Sunday, June 3, 2012

EXCLUSIVE INTERVIEW NA MARIO GOMEZ: SPAIN NA UHOLANZI WANATISHA LAKINI NINA IMANI HUU NI MWAKA WETU

Qn: Unajisikiaje timu yako kupangwa kwenye kundi moja na Ureno na Uholanzi?
"Kushinda vizuri michuano kama hii ni lazima ukutane na timu kubwa na nzuri katika hatua fulani. Michuano ya Euro ni ya kiwango cha juu, hivyo sitegemei kupata ushindi kirahisi. Kwa kuanza tu tutakutana na Ureno na Uholanzi na nategemea kwamba tutakuwa tayari kupambana na kupata matokeo. Hii ndio nguzo ya timu yangu."


TAIFA STARS YAJIPANGA KUIKABILI GAMBIA NYUMBANI


Kikosi cha Taifa Stars ambacho jana kilicheza na Ivory Coast hapa Abidjan na kupoteza kwa mabao 2-0 kinaendelea kujinoa kwa mechi ijayo dhidi ya Gambia itakayochezwa Jumapili (Juni 10 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
 
Kwa mujibu wa programu ya Kocha Kim Poulsen, Taifa Stars imefanya mazoezi leo asubuhi kwenye uwanja wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Ivory Coast (FIF) ambao uko pembezoni mwa jiji la Abidjan.
 
Timu hiyo itafanya tena mazoezi kesho (Juni 4 mwaka huu) asubuhi kabla ya kuanza safari ya kurejea nyumbani saa 1.30 usiku kwa ndege ya Kenya Airways kupitia Nairobi ambapo itawasili Dar es Salaam, Juni 5 mwaka huu saa 1.40 asubuhi.

UAMSHO ZANZIBAR WASALIM AMRI KWA POLISI


Na Mwandishi wa Jeshi la Polisi Zanzibar
Wananchi wa Zanzibar wakiwemo wafuasi wa Kikundi cha Uamsho kilichotangaza kufanyika kwa mhadhara kwenye viwanja vya Lumumba mjini hapa, kimetii amri ya Jeshi la Polisi kwa kutoonekana kwa muumini ama viongozi wa kikundi hicho katika viwanja hivyo.
Afisa Habari Mkuu wa Jeshi la Polisi Zanzibar Inspekta Mohammed Mhina, amesema leo kuwa, Jeshi la Polisi limeweza kudhibiti maeneo mbalimbali ya mji wa Zanzibar na hivyo kutojitokeza tena kwa wafuasi wa kikundi hicho kama ilivyotangazwa awali.
Inspekta Mhina amesema Kikundi hicho cha Uamsho kupitia kwa Kiongozi wake Sheikhe Farid Hadi, juzi kilijigamba kufanya Mhadhara mkubwa leo arasili katika viwanja vya Lumumba mjini hapa hata baada ya Serikali kupiga marufuku mikusanyiko, kimeshindwa kufanya hivyo kufuatia agizo la Jeshi la Polisi lakuwataka wasitishe vinginevyo wangekabiliana na mkono wa dola.
Jana Kamishna wa Polisi Zanzibar CP. Mussa Ali Mussa, alitangaza kuupiga marufuko mhadhara huo na kuwataka wananchi na waumini kutohudhuria na kwa yeyote atakayekaidi agizo hilo angechukuliwa hatua kali.
Kufuatia agizo hilo, Polisi wa Operesheni maalum leo, walimwagwa katika viwanja vya Lumumba huku magari yenye askari wa kutuliza ghasia yakiranda kwa kila eneo kumkabili yeyote atakayekaidi na kufika kwenye viwanja hivyo kwa madhumuni ya kuhudhuria mhadhara huo.
Hatua hiyo ya Polisi imeweza kudhoofisha kabisa hali ya majigambo ya viongozi na wafuasi wa Kikundi hicho cha Uamsho waliotangaza kufanya mhadhara huo hata baada ya serikali kupiga marufuku.
Viongozi wa kikundi hicho ambao walionekana kugawanyika waliwajulisha baadhi ya wafuasi wao kuwa hali isingekuwa swari kwa upande wao kutokana na Jeshi la Polisi kusambaza makachero na askari wa kawaida katika maeneo mbalimbali ikiwemo Viwanja vya Lumumba palipopangwa kufanyika kwa mhadhara huo.
Ni wafuasi wachache tu walionekana kufika katika msikiti wa Mbuyuni kwa sala ya kawaida na pengine kupata taarifa za hatima ya mhadhara huo uliopigwa stop na Jeshi la Polisi.

WAKAZI MBAGALA KIBONDEMAJI WALIA NA DIWANI WAO

 


 WAKAZI wa Kibondemaji Kata ya Mianzini wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam  wamemlalamikia diwani wa kata hiyo, Cecilia Macha (CCM), kwamba ni kikwazo  cha kata hiyo kukosa huduma muhimu kwa jamii ikiwemo Zahanati.
 Wakizungumza kwa nyakati tofauti na fullshangweblog.com leo, Wakazi hao walisema diwani akiwa ndiyo Mwenyekiti wa maendeleo wa Kata, tangu achaguliwe ameshindwa kuitisha mkutano wa aina yeyote, kujadili kero zinazo wakabili  wananchi wa mtaa huo.
Wananchi hao walisema  wanamlalamikia diwani huyo kwakuwa anatambuwa fika kero za mtaa huo, ambapo hakuna shule ya msingi wala sekondari hali inayowafanya watoto kusafiri zaidi ya kilomita 4 hadi sita kwa ajili ya kufuata shule.
Mmoja wa wakazi hao, Halima Juma alisema ukiachilia mbali kukosekana kwa shule, bado akina mama wajawazito wamekuwa wakipata matatizo makubwa kutokana na kukosekana kwa  barabara hali inayofanya usafiri kuwa wakubahatisha pindi wanapotaka kwenda hospitalini wakati  kujifungua.
"Angali  hakuna barabara, maji wala zahanati na kituo cha polisi huduma ambazo ni muhimu katika maisha ya kila siku kwa jamii"alisema Halima.
Naye Christopher John alisema  serikali inapaswa kumchukulia hatua mkandarasi aliyejenga barabara ya mtaa huo kwani ameijenga katika kiwango kisichoridhisha na kusababisha barabara hiyo kuharibika kwa muda mfupi.
Alisema barabara iliyopo hivi sasa imejengwa kwa nguvu za vijana wa mtaa huo ambapo hivi sasa wanachimba mitaro,  iliyojengwa na mkandarasi huyo, imejifukia katika kipindi cha mwaka mmoja tangu kujengwa.
Akijibu malalamiko hayo, diwani wa Kata hiyo, Cecilia alisema serikali haiwezi kujenga hospitali kila mtaa ila hizo ni propaganda "Chamsingi mwandishi  naomba ufike ofisini kwangu nikukonyeshe hali halisi"alisema Cecilia.
Aidha, alisema matatizo mengine yamekuwa yakichangiwa na fungu dogo la pesa za maendeleo zinazotengwa katika wilaya ya Temeke yenye kata 42