Tuesday, June 5, 2012

MANCHESTER CITY KUMTUMA MTU KUIPELEZA STARS

Kachelo wa Man City aipeleleza Taifa Stars

Kalou wa Ivory Coast akichuana na Mwana Samatta wa Taifa Stars

MPELELEZI wa vipaji vya soka toka klabu tajiri England, Manchester City, Joe Mulberry alitua kwa siri mjini Abidjan na kupiga kambi kwenye hoteli ya Ibis Plateau, ambayo pia Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) ilifikia na lengo lilikuwa moja tu kuwachunguza wachezaji wa timu hiyo, Mwananchi limebaini.

Mulberry, raia wa Uingereza mwenye jukumu la kuchunguza vipaji kwa nchi za Afrika Magharibi, alifanya kazi ya kuipeleleza Stars bila kutaka mtu yeyote kufahamu kabla ya mwandishi wa habari hizi kumbaini.

Awali, Mulberry aliyeweka makazi yake nchini Ghana alipanga kwenye chumba namba 604 cha hoteli ya Ibis Plateau.

Baada ya gazeti hili kupata fursa ya kuongea naye muda mrefu, lilimbaini na ndipo naye alipomfichua siri kwamba alikuja Abidjan kwa ajili ya kuangalia pambano la Stars dhidi ya Ivory Coast.
Kwa mujibu wa uchunguzi wake wa haraka, Mulberry alivutiwa na kipaji cha mshambuliaji Mbwana Samata na cha kushangaza katika kipindi kifupi tayari alikuwa amekusanya habari zote za Samata.

Miongoni mwa dodoso muhimu alizokusanya ni pamoja na mabao mawili aliyofunga wakati wa mchezo wa Ligi ya Mabingwa wa Afrika dhidi ya Dynamo ya Zambia na El Merreikh ya Sudan akiwa na timu yake ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Mulberry alikiri Samata alikuwa na kipaji kikubwa lakini akataka amuone zaidi siku za usoni kujua kama alikuwa na uwezo mkubwa wa kufunga kama ilivyo katika kuuchezea mpira.

“Nitasafiri kwenda Ghana kumtazama kwa ajili ya pambano la ligi ya mabingwa kati ya Berekum Chelsea dhidi ya TP Mazembe pale Accra, Julai 5. Kama atakuwa yuko safi tena nitajaribu kuzungumza na timu yake.”

Hata hivyo, Mulberry alisema Samata hawezi kucheza katika Ligi Kuu ya England kwa sasa na badala yake anaweza kupelekwa katika ligi nyingine kabla ya kupata uzoefu wa kucheza ligi kubwa Ulaya. 


Wakati huohuo, msafara Taifa Stars, unatarajiwa kuwasili leo asubuhi na ndege ya Shirika la ndege la Kenya Airways ukitokea mjini Abidjan ilipocheza na kufungwa na wenyeji wao, Ivory Coast kwa mabao 2-0 katika mchezo wa kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia.

Stars ilitarajiwa kuondoka Abidjan jana usiku na kupitia Nairobi usiku wa manane kabla ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere saa moja asubuhi leo.

Kabla ya kuondoka Abidjan, kocha wa taifa Stars alikuwa ameendeleza programu yake ya mazoezi kama kawaida, huku akiwataka wachezaji wa timu hiyo wasizembee katika pambano la Jumapili dhidi ya Gambia.

Mchezaji pekee ambaye alikosekana katika mazoezi ya juzi na jana alikuwa ni mlinzi wa kushoto wa timu hiyo, Waziri Salum ambaye aliumizwa kwa bahati mbaya kifundo chake cha mguu na mlinzi mwenzake, Erasto Nyoni

No comments:

Post a Comment