Tuesday, June 5, 2012

MBOWE:CCM IKISALIMIKA 2015 NAJIUZULU SIASA.

 
MWENYEKITI wa Chadema, Freeman Mbowe (pichani) amesema moto uliowashwa na chama hicho katika Operesheni Sangara utaendelea nchi nzima, lengo likiwa ni kuiondoa CCM madarakani na iwapo itasalimika mwaka 2015, atajiuzulu siasa.

Mbowe alitoa kauli hiyo juzi alipohutubia mamia ya wakazi wa Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara wakati chama hicho kilipofanya mkutano mkubwa kwenye uwanja wa mpira wilayani humo.
Alisema CCM kimepoteza mwelekeo wa kuongoza taifa na ndiyo sababu maisha ya Watanzania yamezidi kuwa mgumu kadri miaka inavyozidi kusonga mbele.

“Wajibu wa Serikali kokote duniani ni moja tu, kuwezesha watu wake kutoka katika hali ngumu za maisha na kuwapeleka kwenye heri, leo CCM wameligawa Taifa katika vipande, wanauza rasilimali za nchi na kuwadidimiza watu wa kipato cha chini wengi wao wakiwa ni wakulima,” alisema Mbowe na kuongeza:

“Ndugu zangu ngojeni niwaulize swali, wakati wa utawala wa Mwinyi na Mkapa (marais wastaafu, Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa), ni kipindi gani maisha yalikuwa mazuri?” Wananchi wakajibu (kipindi cha Mwinyi). Miaka 10 ya uongozi wa Mkapa na miaka saba ya Kikwete, ni kipindi gani maisha yamekuwa magumu zaidi?" Wakajibu (Kikwete); Je, 2015 wanakuja tena kutuomba kura huyo atakayekuja si ndiyo itakuwa mbaya zaidi, Chadema hatuwezi kukubali na moto huu tuliowasha utaendelea nchi nzima hadi Uchaguzi Mkuu wa 2015 na kama CCM itasalimika nitajiuzulu siasa.”

No comments:

Post a Comment